Wednesday, June 28, 2017

Sumatra:Wanaopandisha Nauli Sikukuu Kukiona

Baadhi ya mabasi yakisubiria abiria katika stendi kuu ya mabasi Mkoani Iringa. Imekuwa ni desturi kwa wamiliki wa mabasi kupandisha nauli wakati wa msimu wa skukuu za Krismas na Mwaka Mpya (Picha Na Sabinus Paulo).

Na Stephan Ngolongolo
Mwandishi- Iringa Kwetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imetoa onyo kali kwa wasafirishaji kutokupandisha nauli kulelekea msimu wa sikukukuu za Krismas na Mwaka mpya.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni, Afisa Mfawidhi SUMATRA Mkoa wa Iringa, Ngereza Pateli amesema kuwa kitendo cha kupandisha nauli bila idhini ya mamalaka hiyo ni kinyume na sheria ya usafirishaji.

Aidha afisa huyo amewataka wananchi kutumia namba 15276 ili kupata taarifa zinazohusiana na viwango vya nauli na bei elekezi, huduma ambayo hutolewa na mamlaka hiyo. Ili kupata taarifa, abiria anatakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maandaishi kupitia simu yake ya mkononi kwa kuandika neno nauli, anaacha nafasi, kisha anaandika mahali anapotaka kusafiri kisha anachagua daraja la basi husika na kuutuma ujumbe huo kwenda namba tajwa hapo huu.

“Kupandisha nauli bila idhini ya mamlaka ni kosa kisheria... kwa hiyo nitoe wito kwa wamiliki wa wote mabasi wasifanye hivyo, kwani tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria.” Alisema Pateli.

Afisa huyo aliongeza kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kupandisha bei ya nauli hususani kwa mabasi yanayofanya safari za mikoani wakati wa msimu wa sikukuu. Kwa upande wake, Wakala wa Mabsi ya Delux, Julius Eziudy amesema tatizo la kupandisha bei za nauli wakati wa sikuku limekuwa sugu mkoni Iringa linalosabaishwa na wapiga debe.

Alikiri kuwa mara nyingi msimu wa sikukuu ipo changamoto kubwa ya uhaba wa magari ingawa kwa upande wa kampuni yao wana magari ya kutosha hivyo kuwatoa hofu wateje wao na kuwataka
wafike mapema kukata tiketi. 

“Kama ikitokea magari yetu yote yamejaa huwa tuanomba vibali vya muda mfupi na kutumia magari wa watu wengine kutoa huduma kwa wateja wetu.” Alisisitiza. 

Mwenyekiti wa Umoja waWakatishaji Tiketi stendi kuu ya mabasi mkoani Iringa, Erasto Gasper amesema uzoefu unaonesha baadhi ya abiria wanatambua utaratibu wa kukata tiketi tofauti na hapo nyuma.

Mtalemwa Alex ni kondakta wa mabasi ya Kampuni ya Mwendamseke. Anasema kuwa msimu kama huo ukifika wanapata faida kubwa kutokana na kuwepo kwa abiria wengi hivyo wapiga debe wanalazimika kupandisha nauli bila utaratibu.

Kwa mujibu wa Pateli, SUMATRA kwa kushirikiana na wadau wengine wa usafirishaji kama, polisi wa usalama barabarani wamejipanga kuhakikisha kwamba hakuna adha ya usafiri kuelekea Krismas na mwaka mpya.

“Tumelitambua jambo hilo, hivyo tumejipanga kufanya ukaguzi wa magari kuanzia asubuhi
mpaka jioni.” Aliongeza “Pia tumekuwa tukitoa elimu kupitia vyombo vya habari kuwataka wananchi wakate tiketi kwenye ofisi huska ili kuepusha ulaghai.”

x

No comments:

Post a Comment