Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa tabora Mohamed Kansa |
Kama zilivyo za ndoto za usiku zinapofikia kikomo baada ya pambazuko la alfajiri, ndivyo ilivyo hali ya Igunga sasa. Kwa kawaida hakuna anayependa ndoto tamu ikatizwe, lakini kama ndoto hiyo ni ya kutisha basi muotaji hupata ahuweni pale anapozinduka usingizini na kutambua kumbe ilikuwa ni ndoto.
Ni baada ya kumalizika uchaguzi mdogo kufuatia kujiuzulu kwa Rostam Aziz aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa takribani miaka 17 baada ya kulitwaa mwaka 1994 kufuatia kifo cha Charles Kabeho aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.
Imebakia historia kwa watu wa jimbo Igunga kwani wapo wanaotamani iwapo hekeka za kampeni zingeendelea. Hawa ni pamoja na wafanyabiashara ya nyumba za kulala wageni, mama ntilie, hoteli, vituo vya mafuta, baa, madereva wa taksii na maduka ya kila aina.
Kuna wale waliotamani kuona helikopita za CCM, CUF na CHADEMA zikiendelea kuteka anga la jimbo lao, lakini pia katika vijiwe vya kahawa vilijaza wateja kwa sababu ya gumzo la uchaguzi.
Wapo waliotamani kuendelea kuwaona na kuwasikiliza Dk. Wilbroad Slaa na Freeman Mbowe wa CHADEMA wakijenga hoja za kisiasa jukwaani huku wakipambwa na nyimbo za kuvutia kama ‘People’s Power’
Pia wapo waliopenda kumsikiliza Rais mstaafu Ndugu, Benjamini Mkapa na Ismail Aden Rage na bastora yake kiunoni wakimwaga sera za Chama Cha Mapinduzi kwa ufasaha zaidi huku wakivutiwa na jukwaa la bendi ya TOT na wasanii maarufu kama Ze Orijino Komedi.
Lakini pia wapo wale waliovutiwa sana kusikiliza hotuba ya Ismail Jusa na Julius Matatilo wakimnadi Mgombea wa CUF kwa umakini wa hali ya juu.
Kwa upande wa vyama vya siasa ni furaha kwa CCM waliobahatika kushinda huku huzuni na majonzi yakiviendea vyama vilivyoshindwa katika uchaguzi huu.
Binafsi napenda kuvipongeza vyama vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi huo kwani wametumia haki yao ya kikatiba kuimarisha kidemokrasia nchini.
Katika uchaguzi vyama vinane vilishiriki katika uchaguzi mdogo wa Igunga. Vyama hivyo ni CCM, CHADEMA, CUF, SAU, UPDP, AFP, CHAUSTA na DP.
Wahenga walipata kusema “Chovya chovya humaliza buyu la asali” na mimi leo hii nataka niyatumie maneno haya kama msingi wa makala yangu.
Ninataka kijikita sana katika kutoa tathini ya uchaguzi huku tayari jimbo hilo likiwa limekwisha kuchukuliwa na Chama Cha Mapinduzi ambapo Dk. Dalaly Kafumu ni mbunge mteule kwa mujibu wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Napenda kuzungumzia zaidi vyama vitatu vya CCM, CHADEMA na CUF kwani hivyo ndivyo vyama vilivyoonyesha ushindani mkali ambao haujawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
Kwanza kabisa ninataka nipingane na hoja ya Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye kupitia vyombo vya habari kwamba, vurugu za wafuasi wa CHADEMA zilisababisha watu kutokujitokeza kupiga kura.
Hoja yangu ni kwamba idadi ya wapiga kura katika jimbo la Igunga ni watu 171,019 na watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huu ni watu 53,672 ambayo ni sawa na asilimia 33.3
Ukilinganisha na uchaguzi mkuu wa mwaka jana ni watu wapatao elfu 40 ndiyo walipiga kura ambayo ni sawa na 27 asilimia hivyo mwaka huu kuna ongezeko la takribani asilimia nane.
Kwa mantiki hiyo basi kumbe wapiga kura wameongezeka kwa kuvutiwa na kukiamini Chama cha Demokrasia na Maendeleo ukilinganisha na mwaka jana ambapo CHADEMA haikusimamisha mgombea katika uchaguzi mkuu wa 2010.
Dhana hiyo inajithihirisha kuwa Rostam Aziz hakuwa na mpinzani hivyo wananchi walipuuza kwa kuamini wapige kura wasipige atashinda tuu na hii ndiyo sababu ya wapiga kura kupungua katika uchaguzi wa mwaka jana.
Vilevile kwa mtazamo huo ninadiriki kuamini kwamba kushiriki kwa CHADEMA katika uchaguzi huu kumeongeza idadi ya wapiga kura baada ya kuona kuna mgombea mpya ambaye ni Ndugu Joseph Kashindye wa CHADEMA.
Kwa upande wa CCM sioni kama ni ushindi wa kujivuna kama Nape anavyodai kwamba mkakati wa kukisafisha chama umefanikiwa kwa kuungwa mkono na wananchi wa Igunga.
Tumeshuhudia CCM ikipokonywa na CHADEMA zaidi ya kura elfu 9 ambazo ni sawa na asilimia 22 hivyo si suala la kujivuna kwa ushindi huo ukilinganisha na ushindi wa mwaka jana wa kura elfu 35 sawa na asilimia 72.
Ni wakati wa CCM kukaa chini na kujitathmini upya ili kubaini nini chanzo cha kukosa mvuto kwa wananchi hata kuzidi kushuka siku hata siku, kama mwanzo wa makala yangu nilivyo nukuu maneno ya wahenga “Chovya chovya humaliza buyu la asali” hivyo basi buyu la asali ya CCM linazidi kuisha kwa chovya chovya ya wapinzani.
Kwa upande wa Chama Cha Wananchi (CUF) pia kinapaswa kujitathimini upya ili kubaini nini chanzo cha kufanya vibaya kwenye uchaguzi huu ukizingatia kilikuwa na mtaji wa kura elfu 11 za uchaguzi wa mwaka jana.
Ni wazi kwamba kura hizo si mwingine aliyewapokonya isippokuwa ni CHADEMA. Kama Mtatiro alivyoeleza vyombo vya habari kuwa kuitwa ‘CCM B’ kumekigharimu chama hicho hata kikaanguka kwa kishindo. serikali ya umoja wa kitaifa huko visiwani Zanzibar ndiyo hasa chanzo cha kupoteza kura Igunga.
Yawezekana kabisa CUF ikashindwa kuunguruma tanzania Bara katika uchaguzi ujao hasa ukilinganisha ni kipindi kifupi sana cha umoja huo na CCM.
Kwa CHADEMA pia wanapaswa kupongezwa kwa kazi waliyofanya ndani ya muda mfupi na kupata kura 23,260 ambayo ni sawa na asilimia 44.32. ni vyema sasa wakajitathimini pia ili kubaini ni kasoro gani zilizowanyima ushindi.
Matokeo hayo yamepokelewa na wasomi kwa hisia tofauti tofauti. Tumemsikia Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Benson Bana akisema “matokeo hayo yameonyesha jinsi CCM kinavyozidi kupotea machoni mwa Watanzania”
Dk Bana aliongeza kuwa CCM hakiwezi kutembea kifu mbele wakati wananchi waliomchagua mbunge wa chama hicho hawafiki hata asilimia 50 ya idadi ya waliojiandikisha kupiga kura.
Bana aliongeza kuwa umefika wakati wa CCM kujitazama upya kwa kuwa CHADEMA kinakuja kwa kasi na kimejidhihirisha katika uchaguzi huo nkwa kupata kura nyingi licha ya kuwa hakikuwa na mtandao mkubwa katika jimbo hilo.
“Chadema wameibuka vizuri na wanaendelea kukubalika ila CCM kinazidi kupoteza ushawishi na mvuto wao kwa wananchi” alisema Bana.
Natoa wito kwa wananchi wa Igunga kwamba suala la kupiga kura ni muhimu sana kwa ustawi wa maendeleo ya jimbo lao. Kuchagua kiongozi bora ndiyo msingi wa maisha bora ya wana Igunga.
Hivyo basi, idadi ya watu waliojitokeza (33.3 asilimia) bado ni ndogo japokuwa imeongezeka kidogo ukilinganisha na mwaka jana.
Nawaomba vijana na wazee, wake kwa waume jitokezeni kwa wingi kujiandikisha kupiga kura muda utakapofika ili kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa hili. Ni sisi tukiamua tunaweza kuijenga nchi kupitia viongozi waadilifu.