Wananchi wadai kuchangishwa mbuzi kwa mabavu
Na mwandishi wetu
MBUNGE wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili ameilalamikia Ofisi ya Waziri Mkuu, akisema mtendaji mmoja wa Serikali alikamatwa
kutokana na kushindwa kukusanya mchango wa mbuzi tisa za zawadi kwa
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa ziara yake Wilaya ya Maswa, mkoani
Simiyu.
Kamili aliyasema hayo, wakati akiuliza swali la
nyongeza kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Aggrey
Mwanri baada ya swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Maswa
Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (Chadema), kuhusu mipaka ya madaraka
kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kiutendaji.
Aidha, Kamili aliongeza kusema kuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa aliwaagiza watendaji wote wa
kata kukusanya mbuzi ikiwa ni zawadi za ujio wa Waziri Mkuu katika
wilaya yao na kwamba walioshindwa walikamatwa.
Akijibu swali hilo, Mwanri
alisema ofisi yake haina taarifa ya tuhuma hizo na kumtaka mbunge huyo
azithibitishe. Alisema Serikali haina utaratibu wa kuomba kupewa zawadi
mbalimbali kwa viongozi wake na kama mbunge huyo ana ushahidi wa suala
hilo autoe.
Mara baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne
Makinda alimpa fursa mbunge huyo kueleza kama anao ushahidi huo na
akajibu kuwa anao kwani aliona hata kupitia luninga Waziri Mkuu Pinda
akikabidhiwa zawadi.
Kwa upande mwingine, Kamili aliulizia juu ya operesheni
ya kuhamisha wakazi wa pori la Maswa ambao nyumba zao kadhaa zilichomwa
moto na wafugaji kadhaa kutimuliwa bila kujua pa kwenda.
Akijibu
swali hiyo, Mwanri alisema mgogoro huo wa kuhamishwa wananchi hao,
tayari ulifuatiliwa na Serikali na Waziri wa Nchi, Tamisemi wakati huo,
George Mkuchika alikwenda katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na
kupata taarifa sahihi.
Hata hivyo, alisema wananchi wa vijiji
saba vya eneo hilo, walikubaliana kuanzisha Hifadhi ya Jamii (WMA) na
kutoa eneo hilo kwa mwekezaji jambo ambalo lilitekelezwa.
Awali,
akijibu swali la Kasulumbayi, Naibu Waziri Mwanry alisema wakuu wa mikoa
na wilaya nchini, hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria, kuingilia utendaji
kazi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwa zinatekeleza majukumu yake
kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali.
Kasulumbayi
alitaka kujua inakuwaje wakuu wa mikoa na wilaya ambao kiutendaji ni
watumishi wa Serikali Kuu, wanatoa amri kwa watendaji walio chini ya
wakurugenzi wa wilaya, kuhamisha wananchi katika maeneo yao. Akahoji
mpaka wa madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu unaanzia na
kuishia wapi kiutendaji?
Mwanri alisema mkuu wa mkoa kwa mujibu
wa Sheria ya Tawala za Mikoa Na.19 ya mwaka 1997, katika vifungu Na 5, 6
na 7 ana wajibu wa kusimamia kazi na shughuli zote za Serikali katika
mkoa ikiwa ni pamoja na kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa,
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizotungwa na Bunge.
Alisema majukumu ya wakuu wa
wilaya yametengwa katika kifungu Na.14 (1-3) cha Sheria ya Tamisemi,
Na.19 ya mwaka 1997 kwamba yeye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za
Serikali katika wilaya yake.
“Hivyo madaraka ya jumla ya mkuu wa
wilaya yanatiririshwa kutoka kwa Mheshimiwa Rais kupitia kwa mkuu wa
mkoa, kwa upande wa watendaji walio chini ya mkurugenzi wa halmashauri,
wao ni watekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu zilizopo,” alisema.
Hata hivyo, alisema mipaka
ya madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu imeanishwa katika
Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa Na
19 ya 1997.
“Kwa kuzingatia sheria hizo ni kwamba mkuu wa mkoa na
wilaya anaruhusiwa kuingilia kati inapotokea mamlaka za Serikali za
Mitaa zimeshindwa kutekeleza majukumu yao au kukiuka misingi ya sera na
sheria zilizopo.