Tuesday, October 25, 2011

Mbunge aswekwa rumande kwa kuvamia kituo cha polisi

Mbunge wa Nzega Dk. Hamis Kigwangala

Na Moses Mabula, Nzega

MBUNGE wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangala (CCM) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Wilaya ya Nzega akikabiliwa
na makosa sita yakiwemo kuvamia kituo cha polisi wilayani hapa.

Dkt. Kigwangalla alitiwa mbaroni juzi na Jeshi la Polisi wilayani hapa huku akiwa na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo, Bw. Mrisho Hamisi, Bw. Methew Dotto, Bw. Mwanja mwandu wote wakazi wa Kata ya Nata ambao ni badhi ya wachimbaji wadogowadogo waliokuwa katika vurugu zilizotokea juzi katika Kijiji cha Mwabangu.
 
Wakisomewa mashtaka na Waendesha Mashtaka Merito Ukingoji na Joseph Mbwana, ilidiwa kuwa walifanya mkusanyiko usio halali Oktoba 23 mwaka huu katika mgodi mdogo uliopo kijiji hicho.
 
Kosa la pili na la tatu ni kuingia katika mgodi mdogo unaomilikiwa na wawekezaji bila idhini ya wamiliki na kuvamia Kituo cha Polisi cha Nzega saa mmoja jioni.

Shitaka la nne kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao ni kufanya njama katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya na kufanya maandamano kuvamia Kituo cha Polisi.

Makosa mengine ni kupiga na kujeruhi watu waliotajwa kuwa ni Mosesi
kichambi na Feldinald Yusuph ambao wamejeruhi katika ghasia zilizotokea juzi baada ya wachimbaji wadogo kuchoka kunyanyaswa na kunyang'wanywa eneo lao.

Waendesha mashtaka hao walidai kuwa upelelezi wa tuhuma hizo bado unaendelea kubaini chanzo cha vurugu huku mbunge huyo akiwekewa pingamizi ya kutofika eneo hilo la mgodi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuepusha tafrani inayoweza kujitokeza kwa wananchi na wawekezaji.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega, Ajali Milanzi, watuhumiwa hao walikana mashtaka hayo yote huku mbunge huyo akipewa dhamana baada ya kujidhamini mwenyewe kupitia nafasi yake, kisha kuwadhamini wenzake watatu.

hata hivyo Mahakama hiyo ilimpa dhamana hiyo kwa muda na kumwamuru kuwafikisha mahakamani hapo leo watuhumiwa wenzake aliowadhamini wakiwa na watu watakaowadhamini upya, vinginevyo mahakama hiyo itafuta dhamana kwa watu wote. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Novemba 18, mwaka huu.

Mbunge azungumza
 
Baada ya kuachiwa, mbunge huyo alisema kitendo hicho cha kumweka ndani kimemdhalilisha vya kutosha hasa akiwa katika kudai haki ya wananchi wake ambao wamekuwa wakionewa mara kwa mara na wawekezaji hao.
 
"Nimeshangazwa na Jeshi la Polisi hasa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) kunibambikia makosa ambayo hayana ukweli pamoja na kunidhalilisha kunipiga vibao kama mtoto mdogo na dhihaka mbalimbali kwa wananchi wangu ambao walikuwa wakidai haki yao ya msingi, hii si haki sikutendewa haki katika hili ni uonevu mtupu," alisema Dkt. Kigwangalla.
 
Aliapa kutokata tamaa kutetea haki na maslahi ya wananchi wake licha ya kugeuziwa kibao wakati gari lake lenye namba T 357 BMP aina ya Caldin lilipigwa mawe na kusababisha kuvunjika kioo cha mbele na kupigwa mawe yeye na wananchi wake wakidai haki.
1

No comments:

Post a Comment