Monday, October 17, 2011

Magamba yazidi kuitafuna CCM

Katibu wa itikadi na uenezi CCM Nape Nnauye akihutubia wanachi wa Mwanza


Mwanza

 FALSAFA ya kuvuana magamba nchini ya Chama Cha mapinduzi (CCM) imezidi kukitesa
chama hicho na kuzua mvutano baina ya viongozi na baadhi ya wanachama sasa ikielezwa kuwa lazima mageuzi hayo yaendelee vinginevyo hali itakuwa mbaya na nchi itashindwa kutawalika.

Wakati kumekuwapo na msuguano na maelezo kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye anapotosha maagizo ya chama chake kuhusu dhana hiyo, yeye ameibuka na kusema mageuzi yanayoendelea ndani ya chama hicho maarufu kama kujivua gamba ni ya kweli, na yakifanyika ipasavyo ni ukombozi kwa wananchi wanyonge wa Tanzania lakini machungu kwa kundi linalofaidika na jasho lao.

Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara jijini Mwanza jana kwenye viwanja vya Magomeni, Kirumba, Bw. Nnauye alisema mageuzi hayo ni ukombozi kwa wanyonge kwa kuwa yamelenga kuimarisha misingi ya uadilifu na kuwajibika kwa viongozi waliopewa dhamana.

"Ni rahisi leo kumkuta kiongozi anamiliki utajiri wa kutisha na kufuru kuliko hata kipato chake halali, tukisema tukae kimya nchi hii haitatawalika. Dawa ni kufanya mageuzi haya leo kabla hali haijachafuka sana," alisema na kuongeza.

Kwa mujibu wa Bw. Nnauye, kufanikiwa kwa mageuzi hayo kutasaidia kuhakikisha kunakuwapo mgawanyo mzuri wa rasilimali za nchi, hivyo kulewa ukombozi wa moja kwa moja kwa wanyonge nchini.

"Tusisahau ndugu zangu, nguvu ya chama hiki na heshima yake imekuwa ni kutetea wanyonge nchini, Afrika na duniani kwa ujumla. Kutetea wanyonge lazima uhakikishe rasilimali za nchi zinanufaisha wanyonge, bila uadilifu na kuwajibika haitawezekana, ndio malengo ya mageuzi tuyafanyayo," alisema Bw. Nnauye.

Alisisitiza kuwa misingi ya CCM na imani yake vikifuatwa na kusimamiwa vizuri kwa dhati bila unafiki kelele zinazosikika leo za matumizi mabaya ya rasilimali za nchi hazitakuwepo na kuweka wazi kuwa kundi linalofaidika na hali ya sasa, ndilo linalopotosha maana ya mageuzi hayo kwa kutoa hoja alizoita dhaifu.

Alisema kumejengeka utamaduni na hasa kwa baadhi ya watu wenye dhamana kujijali wao wenyewe zaidi kuliko wananchi wanaowaongoza, tabia ambayo imeongeza tofauti ya kipato kati ya wananchi wa chini na viongozi wao, huku wengine wakiwa na kipato kisichokuwa na maelezo sahihi.

"Mwalimu (Nyerere) aliwahi kuwahoji viongozi waliotaka uongozi wa juu wakati huo, kwa umri wenu na kipato chenu mmetoa wapi utajiri huu? Na hiyo ilitosha kumzuia mtu asigombee uongozi, leo ukihoji uadilifu wa baadhi ya viongozi utaandamwa wewe, usipokuwa makini wanakutoa roho," alisisitiza Bw. Nnauye.

Akitoa ufafanuzi zaidi Bw. Nnauye alionya kuwa kama tofauti ya kipato isiposhughulikiwa mapema na hasa kuwadhibiti wale wanaojilimbikizia mali kwa njia haramu wakiwemo viongozi na kugeuza chama kichaka chao, nchi itavurugika kwa kuwa wanyonge ni wengi na watatumia nguvu kudhibiti rasilimali zao na kudai usawa.
0

No comments:

Post a Comment