Mwenyekiti wa
kijiji cha Miswechini wilayani Kibaha (mwenye kofia) bwana Dunia Mrisho akiwa
na mkurugenzi mtendaji wa TCIB bwana Deus Kibamba (katikati) wakimgawia machapisho mwana kijiji wa Miswe wakati wa
ufunguzi wa ofisi ya kituo cha taarifa kijijini hapo juzi. (Picha na Elisha
Magolanga)
|
Na Elisha Magolanga
Kibaha.
Jamii kubwa ya watanzania waishio
vijijini wanakabiliwa na tatizo la kukosa taarifa nyingi za kijamii hususani
zile zinazohusu maendeleo na maisha yao ya kila siku.
Akizungumza na
wanakijiji wa Miswechini kata ya Mbwawa wilayani Kibaha wakati wa uzinduzi wa
kituo cha taarifa vijijini, Mkurugeni wa Kituo cha taarifa kwa wananchi (TCIB),
bwana Deusi Kibamba alisema kupata taarifa ni haki yakila mtanzania bila kujali
mahali anakoishi, umri na jinsia ya mtu.
Bwana Kibamba
alisema kuwa kituo kilichofunguliwa kijijini hapo kituo kitatoa fulsa kwa wana
kijiji kujipatia taarifa mbalimbali za kijamii, za kisheria na habari kuhusu mambo
mbalimbali yanayotokea nchini.
“Wanakijiji katika
kituo hiki watapata fursa ya kujisomea majarida, magazeti na tafiti mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kutazama luninga na kufanya majadiliano ya pamoja hapa kituoni,”
alisema Kibamba.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Dunia Mrisho aliwataka wanakijiji wote watumie
vizurifursa iliyotolewa na TCIB kwa ajiliya kujiongezea maarifa ili
waweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kijiji na taifa kwa
kufuatilia kwa ukaribu mambo mbalimbali yanayowahusu.
Akiongelea malengo
ya kituo cha taarifa vijijini, mratibu wa mradi huo, Obeid Mkina alisema kuwa
upatikanaji wa taarifa sahihi unamfanya
mwananchi kuwa na ufahamu wakutosha juu ya masuala mabalimbali
yonayoizunguka jamii yake hivyo hujiamini na kushiriki kikamilifu katika
maendeleo ya jamii.
Mkina aliongeza
kuwa mradi huo wa taarifa vijijini ni miongoni mwa miradi mingine minne inayodhaminiwa
na TCIB katika vijiji vilivyoko Mwanhuzi na Meatu mkoani Simiyu, Kitonga mkoani
Iringa na Micheweni visiwani Pemba ambapo kila kituo kimepewa luninga na
king’amuzi, magazeti, majarida ya taarifa za afya na machapisho ya katiba.