Wednesday, June 28, 2017

Mpango wa Elimu Bure Waibua Mapya Iringa

Baadhi ya wanafunzi wa Secondary mkoani Iringa wamemebeba komputer kuelekea darasa maalumu kwa ajili ya kujifunza. Tanzngu mpango wa Elimu Bure uanzwe kutekelezwa mkoani hapa zipo chngamoto kadha wa kadha zimeanza kujitokeza.


Na Mwanaidi Waziri, Joan Victor

Waandishi-Iringa Kwetu

Utekelezaji wa mpango wa elimu bure uliotolewa na Rais John Magufuli umeibua changamoto kadhaa licha ya kuwa na faida nyingi ikiwamo ongezeko la wanafunzi mashuleni na kupunguza mzigo kwa wazazi masikini nchini.

Haya yamebainika kufuatia wazazi wengi kutoonesha ushirikiano wowote katika masuala ya kielimu
yanayowahusu watoto wao kwa kile wanachodai serikali ndio inashughulikia masuala yote ya elimu hivi sasa kutokana na tamko lake la elimu bure.

Aidha imeonekana kuwa walimu wamekuwa wavivu na kutokuwa makini mashuleni tangu kuanzishwa kwa mpango huo jambo ambalo wazazi wengi wamelilalamikia na kuiomba serikli kushughulikia hali hii kwani inaathiri maendeleo ya watoto kielimu.

Akizungumza na Iringa Kwetu hivi karibuni, Mkurugenzi wa manispaa ya Iringa Ndugu William Mafwele, amesema suala zima la elimu bure lina faida na changamoto zake kutokana na vile baadhi ya watu walivyolipokea na kulitafsiri katika jamii.

Mkurugenzi ameelezea mchakato mzima wa mpango huo ulivyoanza akisema: “Tulilipokea vizuri tamko la Mhe. Rais na mchakato wa utekelezaji wake ulienda vizuri kwa kiwango cha wanafunzi kuongezeka kwa asilimia 68 na ufaulu pia unaongezeka kufuatia watoto wengi kuhudhuria mashuleni bila kubughudhiwa ada ya aina yeyote.”

Kwa upande mwingine, ameongelea changamoto mbali mbali ambazo zinatokana na mpango huu wa elimu bure ikiwemo wazazi kubweteka na kutokutaka kushiriki chochote katika masuala ya maendeleo ya elimu kwa vile serikali imesema “elimu bure”.

Muhadhili wa Chuo Kikuu cha Iringa na mtaalamu wa mambo ya elimu, Dk. Lucas Mwaombela amesema wazo la serikali kuanzisha mpango wa elimu bure ni jema kwani limelenga kuhakikisha kila mtanzania mwenye umri wa kwenda shule anapata elimu bila kikwazo.

Ingawa mpango huu umeonesha kuwepo changamoto mbalimbali zinazoikabili “elimu bure”, Dk Mwaombela anasema “Kila mpango mzuri unazalisha changamoto” na kuongeza kuwa kuwa serikali umeonyesha juhudi kubwa katika kukabiliana na changamoto hizo.

Wito wangu kwa serikali na wadau wote wa elimu nchini, jambo la elimu sio suala la serikali peke yake, tunapaswa kujitoa kuchangia elimu lakini pia serikali itoe ajira za walimu maana tuna walimu wa kutosha wapo mtaani wakisubiri ajira.

Kaimu Afisa wa Elimu Manispaa ya Iringa mjini ambaye hakutaka jina lake litajwe aliongeza kuwa suala la elimu bure limesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi kitu ambacho kimepelekea walimu
kupunguza mitihani mashuleni kuepuka kazi nyingi suala ambalo linapunguza umakini wa wanafunzi katika masomo.

Gazeti la Iringa Kwetu limeshuhudia baadhi ya wazazi wakilalamikia mpango huo kwa kile wanachodai umepunguza umakini wa walimu mashuleni ukilinganisha na hapo awali suala ambalo serikali hailiangalii kwa umakini.

Beti Chengula, ambaye ni mfanya biashara katika soko kuu la manispaa ya Iringa ameliambia gazeti hili kuwa mpango wa elimu bure si mzuri kwasababu walimu hawafanyi kazi kwa bidii tangu uanzishwe na hawapo makini katika ufundishaji wala usimamizi wa watoto mashuleni.

Ameongeza kuwa tangu serikali ianzishe mpango huu, maendeleo ya mtoto wake si mazuri ukilinganisha na hapo awali yalivyokuwa na ndio sababu yeye haoni faida ya elimu kuwa bure na kutoa rai kwa walimu kufundisha kwa moyo kama inavyotakiwa kwa kuwachukulia wanafunzi
kama watoto wao.

Licha ya changamoto mbalimbali zinazotokana na mpango huu wa elimu bure wa serikali, Iringa
Kwetu imeshuhudia baadhi wa wazazi wakiipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua iliyoifikia ya kuifanya.

No comments:

Post a Comment