Saturday, February 16, 2013

TCIB yazindua kituo cha taarifa vijijini

Mwenyekiti wa kijiji cha Miswechini wilayani Kibaha (mwenye kofia) bwana Dunia Mrisho akiwa na mkurugenzi mtendaji wa TCIB bwana Deus Kibamba (katikati) wakimgawia  machapisho mwana kijiji wa Miswe wakati wa ufunguzi wa ofisi ya kituo cha taarifa kijijini hapo juzi. (Picha na Elisha Magolanga)

Na Elisha Magolanga

Kibaha. Jamii kubwa ya watanzania  waishio vijijini wanakabiliwa na tatizo la kukosa taarifa nyingi za kijamii hususani zile zinazohusu maendeleo na maisha yao ya kila siku.

Akizungumza na wanakijiji wa Miswechini kata ya Mbwawa wilayani Kibaha wakati wa uzinduzi wa kituo cha taarifa vijijini, Mkurugeni wa Kituo cha taarifa kwa wananchi (TCIB), bwana Deusi Kibamba alisema kupata taarifa ni haki yakila mtanzania bila kujali mahali anakoishi, umri na jinsia ya mtu.

Bwana Kibamba alisema kuwa kituo kilichofunguliwa kijijini hapo kituo kitatoa fulsa kwa wana kijiji kujipatia taarifa mbalimbali za kijamii, za kisheria na habari kuhusu mambo mbalimbali yanayotokea nchini.

“Wanakijiji katika kituo hiki watapata fursa ya kujisomea majarida, magazeti na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutazama luninga na kufanya majadiliano ya pamoja hapa kituoni,” alisema Kibamba.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Dunia Mrisho aliwataka wanakijiji wote watumie vizurifursa  iliyotolewa  na TCIB kwa ajiliya kujiongezea maarifa ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kijiji na taifa kwa kufuatilia kwa ukaribu mambo mbalimbali yanayowahusu.

Akiongelea malengo ya kituo cha taarifa vijijini, mratibu wa mradi huo, Obeid Mkina alisema kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi unamfanya  mwananchi kuwa na ufahamu wakutosha juu ya masuala mabalimbali yonayoizunguka jamii yake hivyo hujiamini na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Mkina aliongeza kuwa mradi huo wa taarifa vijijini ni miongoni mwa miradi mingine minne inayodhaminiwa na TCIB katika vijiji vilivyoko Mwanhuzi na Meatu mkoani Simiyu, Kitonga mkoani Iringa na Micheweni visiwani Pemba ambapo kila kituo kimepewa luninga na king’amuzi, magazeti, majarida ya taarifa za afya na machapisho ya katiba.