Sunday, October 9, 2011

Hali ya Dr. Mwakyembe yaleta utata

Naibu Waziri wa Ujenzi Dr. Harrison Mwakyembe
Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, amekuwa na hali tete kiafya baada ya kuugua ugonjwa uliomsababisha kuvimba mwili wote.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na yeye mwenyewe zinaeleza kuwa, alianza kuwashwa ngozi miezi mitatu iliyopita kabla ya hali kubadilika siku za karibuni na hatimaye kuvimba sehemu kubwa ya mwili wake.

Mwakyembe alilieleza gazeti hili jana kuwa, baada ya  hali yake kubadilika alianza kupata matibabu katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam akiwa nyumbani kwake Kunduchi Beach.Akizungumza na gazeti hili kwa shida, Dk Mwakyembe alisema hajui chanzo cha ugonjwa huo wa ngozi, daktari wake ndiye anaweza kuelezea kwa usahihi.

“Ni kweli naumwa nipo nyumbani, hata sura yangu imebadilika. Sasa hivi namsubiri daktari wangu, nilisikia natakiwa kupelekwa India kwa matibabu, nasubiri kauli yake si mimi niamue,” alisema na kuongeza;

“Siwezi kusema nimelishwa sumu, ninachosema mimi nimevimba kweli mwili mzima naumwa kweli hapa nimelala na sijui umenipataje kwa simu kwa sababu huwa siiwashi muda huu una bahati kweli”alisema Mwakyembe.

Mke wa Dk Mwakyembe  Mkewe Linah Mwakyembe alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Jumapili, alisema kwa mujibu wa daktari wake, Dk mumewe  anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis.
 “Alianza kuugua muda mrefu kidogo, kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya zaidi,” alisema.

Alisema madaktari waliomfanyia uchunguzi kwa nyakati tofauti katika kipindi hicho walitoa majibu tofauti na kuongeza kuwa wapo waliosema hali hiyo ilisababishwa na kisukari na mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kulikuwa na chembechembe za sumu katika damu yake.

“Baada ya ngozi yake kubadilika sana na hali kuwa mbaya, tulienda hospitali na madaktari walitupa majibu tofauti, wapo waliosema ni kisukari na kuna mwingine alisema kuna chembechembe za sumu,” alisema Linah na kufafanua  kuwa daktari aliyedai hivyo hakuwapa maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa Linah, ngozi ya Dk Mwakyembe inawasha na inakuwa kama inatoa mba mwili mzima hadi kichwani.

Aliongeza kuwa daktari wake ameshauri ufanyike uchunguzi wa kina zaidi ili kujua kama atahitajika kupatiwa matibabu nje ya nchi.